Familia za wahanga wa mauaji ya Tiananmen nchini China wamefanya kumbukumbu ya miaka 30 tangu ukandamizaji huo wa vuguvugu la demokrasia ulipofanyika.
Familia hizo zimeitaka serikali ya China kukubali yaliyotokea na kuwaadhibu waliohusika. Kiongozi wa wanafunzi, Wu'er Kaixi ametoa wito wa vikwazo vya kimataifa dhidi ya tabaka la viongozi wa kikomunisti wa China. Watu wengi waliuawa Juni 4 mwaka 1989, pale jeshi la China lilipotumia vifaru dhidi ya wanafunzi waliokuwa wakidai mabadiliko na demokrasia zaidi katika viwanja vya Tiananmen. Umoja wa Ulaya umetoa wito wa kuwepo uchunguzi wenye uwazi kuhusu mauaji hayo, nayo Marekani imeelezea mshikamano na familia ambazo bado zinaomboleza wapendwa wao waliopoteza maisha katika ukandamizaji huo. China inasema miito ya pande hizo ni kisingizio cha kuingilia katika mambo yake ya ndani.
CHANZO: Idhaa ya Kiswahili DW