Star Tv

Polisi nchini Haiti imesema imemkamata raia wa nchi hiyo aliyetumia ndege binafsi kushirikiana na watu wanaotuhumiwa kupanga na kutekeleza mauaji ya Rais wa Haiti, Jovenel Moise.

Mkuu wa Polisi wa Haiti, Leon Charles amemtambulisha mtuhumiwa huyo kama Christian Emmanuel Sanon, mwenye umri wa miaka 63 anayeishi Florida, Marekani.

Amesema alikwenda Haiti kwa kutumia ndege binafsi mwanzoni mwa mwezi Juni akiwa na walinzi binafsi na alitaka kuchukua nafasi ya urais.

Mkuu huyo wa polisi hakueleza nia ya Sanon, zaidi ya kusema zilikuwa kisiasa na kwamba aliwasiliana na mtuhumiwa mmoja baada ya kukamatwa.

Charles amewaambia waandishi habari kwamba nia ya washambuliaji hao awali ilikuwa kuhakikisha usalama wa Sanon, lakini baadae lengo lilibadilishwa na walimpa mmoja wa wauaji hati ya kumkamata rais na kwamba maafisa wa polisi walipata vitu kadhaa kwenye nyumba ya Sanon.

''Ndani ya nyumba ya Christian Emmanuel Sanon, tumepata kofia yenye nembo ya Mamlaka ya Kupambana na Biashara Haramu ya Madawa nchini Marekani, DEA, masanduku sita ya kuwekea bunduki, maboksi 20 yenye risasi, vibao vinne vyenye namba za magari zilizosajiliwa kwa namba za Jamhuri ya Dominika, magari mawili na mawasiliano aliyofanya na watu wasiojulikana,"- Alifafanua Charles.

Charles amesema jumla ya raia 26 wa Colombia wanatuhumiwa kumuua Rais Moise Jumatano iliyopita, 18 kati yao wamekamatwa pamoja na raia wawili wenye uraia wa Haiti na Marekani.

Amesema bado wanaendelea kuwasaka watuhumiwa watano na kwamba watuhumiwa watatu wameuawa.

Mkuu huyo wa polisi wa Haiti amesema wanashirikiana na maafisa wa ngazi ya juu wa Colombia kubaini taarifa zaidi za wanaotuhumiwa kupanga mauaji hayo, na kuangalia lini waliondoka Colombia na nani alilipia tiketi zao.

Wakati huo huo, kundi la watu wanaotuhumiwa kwa mauaji ya Rais Moise limewaambia wapelelezi kwamba walitaka kumkamata kiongozi huyo na sio kumuua.

Hayo yamebainika katika ripoti iliyotolewa siku ya Jumapili na gazeti la Marekani la Miami Herald. Ambalo liliwanukuu watu waliozungumza na watuhumiwa 19 wanaoshikiliwa hadi sasa, gazeti hilo limeeleza kuwa lengo lao lilikuwa kumkamata Moise na kumpeleka kwenye Ikulu ya rais.

Latest News

Mgogoro wa Maji unatishia Amani Duniani, inasema ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa...
21 Mar 2024 14:18 - Kisali Shombe

Siku ya Maji Duniani ambayo inafanyika tarehe 22 Machi ikiwa na kaulimbiu: 'Maji kwa Ustawi na Amani. Ambapo maji ni moj [ ... ]

Matarajio katika mkutano wa BRICS nchini Afrika Kusini, Jumanne tarehe 22/2023
21 Aug 2023 12:14 - Kisali Shombe

Mkutano huo ambao utafanyikia Johannesburg nchini Afrika Kusini siku ya Jumanne, tarehe 22 Agosti 2023, unatarajiwa kuhu [ ... ]

Rais Ramaphosa Kuwa Mwenyeji wa Rais Xi Jinping wa China
21 Aug 2023 11:11 - Kisali Shombe

Rais Cyril Ramaphosa Jumanne ya tarehe 22 Agosti 2023, atakuwa mwenyeji wa Mheshimiwa Rais Xi Jinping wa China katika Zi [ ... ]

Other Articles

Social Media

Copyright © 2024 . Star Tv - Tanzania. All Rights Reserved.