Aliyekuwa rais wa Sudan Omar al-Bashir alionekana hadharani jana Jumapili, kwa mara ya kwanza tangu kupinduliwa na jeshi Aprili 11.
Bashir alisafirishwa kutoka gereza la Kober mjini Khartoum hadi ofisi ya mwendesha mashtaka kukabiliana na shutuma za ufisadi. Mwendeshamashtaka Alaeddin Dafallah aliwaambia waandishi wa habari kwamba kiongozi huyo wa zamani anashtakiwa kumiliki fedha za kigeni kinyume cha sheria, ubadhirifu na kupokea zawadi kwa njia zisizo halali. Utawala wa miongo mitatu wa Bashir uliangushwa na jeshi baada ya maandamanano ya miezi kadhaa, kupinga kupanda kwa bei ya chakula na kudhoofika kwa uchumi. Mwezi Mei alishtakiwa kuhusika katika mauaji dhidi ya waandamanaji, na polisi ilisema ilikuta nyumbani kwake fedha taslimu katika sarafu mbali mbali, zenye thamani jumla ya dola milioni 100 za kimarekani.
CHANZO: Idhaa ya Kiswahili DW