Makundi ya upinzani nchini Sudan leo yameanza kampeini ya kitaifa ya kutotii sheria baada ya viongozi wake wawili kuripotiwa kukamatwa. Kupitia ujumbe uliotumwa katika mtandao wa Twitter na muungano wa wataalam wa Sudan-SPA- kundi kuu katika upinzani, mgomo huo ni njia ya amani ya upinzani.
Kundi hilo la SPA limesema kuwa ni maafisa wa matibabu na afya pekee ambao hawapaswi kushiriki katika mgomo huo kuhakikisha kuwa wagonjwa na majeruhi wanapata huduma bora. Mgomo huo unajiri siku moja baada ya viongozi wawili wa upinzani kuripotiwa kukamatwa saa chache baada ya kukutana na waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed aliye ziarani nchini humo katika juhudi za kutatua mzozo huo.
CHANZO: Idhaa ya Kiswahili DW