Rais wa zamani wa Afrika Kusini Jacob Zuma ametakiwa mpaka kufikia Jumatano awe amependekeza adhabu ambayo mahakama kuu ya nchi hiyo inapaswa kutoa ikiwa atapatikana na hatia ya kudharau.
Adhabu hiyo inahusiana na kupuuza kwake wito wa kufika mbele ya tume ya uchunguzi inayoongozwa na Jaji Ray Zondo kujibu tuhuma za ufisadi ambazo amekuwa akikana.
Mwezi Januari, mahakama ya katiba ya nchi hiyo ilimwamuru afike mbele ya tume hiyo, lakini akapuuza agizo hilo.
Mwezi uliopita, tume hiyo iliitaka mahakama imhukumu rais huyo wa zamani kwa miaka miwili, ili kuonesha uzito wa vitendo vyake akivyovitenda wakati akiwa madarakani.
Mahakama hata hivyo ilizuia uamuzi katika kesi hiyo, Ambapo wakati huo Zuma alisema haogopi kwenda gerezani ikiwa mahakama zitaamua hivyo.
Wakati huo huo mahakama ya rufaa Jumanne ilitetea uamuzi wa awali kwa serikali kupata pesa ambazo ilikuwa imezitumia kwa ada ya kisheria ya rais wa zamani.
Aidha, inakadiriwa kuwa serikali ililipa kati ya dola milioni moja na milioni 2.2 kama gharama katika kesi hiyo.
CHANZO:BBCSwahili