Rais Uhuru Kenyatta ametangaza mipango ya kusaidia biashara na raia wa Kenya kusonga mbele katika kipindi hiki cha mdororo wa kiuchumi kwasababu ya janga la virusi vya corona.
Hayo yamejiri wakati rais akihutubia taifa kutoka Ikulu ya rais, Nairobi na kusema kwamba mipango hiyo itagharimu shilingi bilioni 53.7.
Katika hotuba yake, rais amesema pesa hizo zitagawanywa katika sekta muhimu kama vile miundombinu, elimu, biashara ndogondogo na za wastani, afya, kilimo, utalii, mazingira na viwanda vya uzalishaji.
Aidha, rais amesema kuwa taifa hilo haliwezi kuendelea kuchukua hatua za kusalia ndani milele;''Sisi kama serikali, kama serikali zingine, mataifa yote dunia zimeanza kuona, hatuwezi kuendelea kusema wakenya tukae nyumbani, hatuwezi kuendelea kusema tu wakenya msiende kufanya biashara, musiende makazi, namna hio".
Taifa hilo la Kenya inachukua hatua sawa na zile ambazo pia zimechukuliwa na nchi nyengine kama hatua ya kuchechemua uchumi unaoendelea kudidimia.
Uhuru amesema hayo wakati ambapo pia alitangaza kuwa Kenya maambukizi 31 ya virusi vya corona na kufikisha idadi hiyo hadi 1192.
Aidha ametoa wito kwa Wakenya ambapo amesema kuwa “Mimi sina shaka Wakenya tukishirikiana, tuungane pamoja, tutashinda huu ugonjwa, lazima tukumbuke ya kwamba jukumu ni letu sisi sote''.
Rais uhuru amewaambia wananchi wake kuwa ikiwa wataendelea kutekeleza masharti yaliyowekwa bila shaka taifa hilo litafanikiwa kukabiliana na changamoto zilizopo kwa sasa.