Ofisi ya Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson ya Downing Streeet imeeleza kuwa Waziri huyo amelazwa hospitalini ili kufanyiwa vipimo vya virusi vya Corona, siku 10 baada ya kukutwa na virusi vya ugonjwa huo.
Taarifa kutoka ofisi hiyo zimeeleza kuwa Boris alikimbizwa katika hospitali moja ya mjini London siku ya Jumapili kutokana na kuonyesha dalili za virusi hivyo ikiwemo kiwango cha juu cha joto mwilini.
Kulingana na Mhariri wa BBC anayesimamia maswala ya kisiasa Laura Kuenssberg amesema Waziri Mkuu huyo anatarajiwa kulazwa hospitalini kwa kueendelea kufanyiwa vipimo vya kawaida.
Katika taarifa ya msemaji wa ofisi ya Waziri Mkuu alisema:”Waziri Mkuu anaendelea kuwa na dalili za virusi vya corona siku chache baada ya kukutwa na virusi hivyo”.
Amesema pia Waziri Mkuu ameishukuru idara ya afya NHS kwa kazi nzuri na kuwaomba raia wa Uingereza kuendelea kufuata ushauri wa serikali wa kusalia nyumbani, ili kuwalinda wafanyakazi wa Afya na kuokoa maisha yao kwa ujumla.
Boris atafanyiwa vipimo kifuani na mapafu yake ili kufahamu iwapo amekuwa akipata tatizo la kupumua na pia huenda akafanyiwa vipimo vya moyo wake pamoja na vipimo vingine kuhusu kiwango cha oksijeni mwilini na kile cha seli nyeupe za damu , ini na figo kabla ya kutolewa hospitalini.
Waziri Boris alionekana hadharani mara ya mwisho akiwasifu wafanyakazi wa huduma ya Afya na wafanyakazi wengine muhimu katika nyumba yake huko Downing street siku ya Alhamisi jioni kabla ya kuongoza mkutano wa virusi vya corona akiwa karantini siku ya Ijumaa.
Mwisho.