Vikosi vya polisi nchini Misri vimetawanywa kwa wingi katika eneo la kati la mji mkuu Cairo na kuzifunga njia zote za kuingia katika uwanja mashuhuri wa Tahriri, kufuatia wito wa maandamano dhidi ya rais Abdel Fattah al Sissi. Wito huo unafuatia tuhuma za rushwa ambazo rais Al Sissi anazikanusha.
Maandamano yameanza Septemba 20 mjini Cairo na katika miji mengine kadhaa kufuatia miito ya mtandaoni ya kuandamana kulaani rushwa katika familia ya al Sissi na jeshi lenye nguvu nchini humo. Rais al Sissi amerejea nyumbani akitokea New York, Marekani ambako alihudhuria Hadhara Kuu ya Umoja wa Mataifa. Akizungumza na umati wa watu waliofika uwanjani kumlahiki, rais al Sissi amewasihi wasitaharuki. Ameitaja risala iliyoenea mtandaoni na kumhusisha na rushwa kuwa ni uongo mtupu. Tangu maandamano ya mwishoni mwa wiki iliyopita kamata kamata inaendelea. Makundi yanayopigania haki za binaadam yanasema watu wasiopungua 2,000 wametiwa ndani hadi sasa.
CHANZO: Idhaa ya Kiswahili DW