Umoja wa Mataifa umeionya Msumbiji kwamba huenda mvua kubwa na upepo mkali unaovuma vikasababisha mafuriko katika siku zijazo wakati ambapo kimbunga Kenneth kinasonga taratibu katika maeneo ya ndani ya nchi hiyo.
Kulingana na shirika la hali ya hewa nchini Msumbiji, kufikia mchana wa jana upepo uliokuwa unavuma kwa kasi ya kiliomita 160 kwa saa ulikuwa umepunguza kasi yake hadi kilomita 70 kwa saa. Lakini mvua kubwa zinatarajiwa kuendelea kunyesha wikendi hii. Shirika la Umoja wa Mataifa la chakula duniani WFP limesema katika baadhi ya sehemu siku chache zijazo huenda kukashuhudiwa kiasi mara mbili cha mvua iliyonyesha wakati katika mji wa Beira wakati wa kimbunga Idai kilichoipiga nchi hiyo mwezi Machi. Mtu mmoja ameripotiwa kufariki dunia katika mkoa wa Cabo Delgado baada ya kuangukiwa na mti.
CHANZO: Idhaa ya Kiswahili DW