Wakati hekaheka za maandalizi kuelekea michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara ikiendelea kwa vikosi 20 vitakavyoshiriki ligi hiyo, Klabu ya Yanga iliyoweka kambi Mkoani Morogoro, imetangaza kuvunja mkataba na aliyekuwa golikipa namba moja wa kikosi hicho Mcameroon Youthe Rostand.
Awali, Viongozi wa klabu hiyo walipanga kumpeleka kwa mkopo klabu yake ya zamani ya African Lyon itakayoshiriki ligi kuu msimu ujao, lakini kabla dili hilo halijakamilika Rostand akaomba kuvunjwa kwa mkataba wake uliosalia mwaka mmoja akieleza kusumbuliwa na matatizo ya kiafya hivyo hatoweza kukitumikia kikosi hicho kikamilifu, taarifa iliyothibitishwa na Afisa Habari wa klabu hiyo Dismas Ten.
Rostand anakuwa mchezaji wa tatu kuondoka klabuni hapo kabla ya msimu kuanza akitanguliwa na mshambuliaji Obrey Chirwa na beki wa kulia Hassan Kesy, huku hali ya kiuchumi ndani ya klabu hiyo ikielezwa kuwa taabani kufuatia siku chache zilizopita Kaimu Katibu Mkuu wake Omary Kaaya kutangaza kutembeza bakuli kuomba michango kutoka kwa wanachama na mashabiki ili kukinusuru kikosi hicho kinachoshiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.