Meneja wa Arsenal Arsene Wenger amesema viwango vya usimamizi wa mechi katika Ligi Kuu England vimeendelea kudorora mwaka baada ya mwaka.
Hii ni baada ya klabu yake kulazwa 3-1 na Manchester City mechi ya Ligi Kuu England Jumapili .
Wenger anaamini mshambuliaji wa City Raheem Sterling alijiangusha na kupewa penalti ambayo iliwasaidia wenyeji kupata bao la pili.
Kadhalika, anaamini bao la tatu halikufaa kukubaliwa kwani lilikuwa la kuotea.
"Nafikiri waamuzi hawafanyi kazi ya kutosha," amesema Wenger.
"Viwango vinashuka kila msimu kwa sasa, na kwa jumla, haikubaliki."
Mambo yakiwa 1-0, refa Michael Oliver aliwazawadi City baada ya Sterling kuanguka alipokabiliwa na Nacho Monreal wa Arsenal.
Sergio Aguero alifunga penalti hiyo.
Baada ya Alexandre Lacazette kukombolea Gunners bao moja, Gabriel Jesus alifungia City bao la tatu lakini David Silva alikuwa amejenga kibanda ardhi ya Arsenal.