Rais wa Marekani Donald Trump amemuomba Rais wa Rwanda Paul Kagame ambaye kwa sasa ndiye mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU) kufikisha salamu zake kwa viongozi wengine wa mataifa wanachama wa AU. Viongozi hao wawili wamekutana mjini Davos, Uswizi pambizoni mwa mkutano wa viongozi na watu mashuhuri kuhusu uchumi na biashara duniani. Mkutano huo wa Kagame na Trump umetokea wiki chache baada ya kiongozi huyo wa Marekani kuyaeleza mataifa ya Afrika kama "machafu" au mataifa ya "mabwege". Hatua hiyo ilimfanya kushutumiwa vikali na viongozi wa AU na baadhi ya viongozi wa nchi za Afrika kama vile Botswana na Ghana. Bw Trump amekanusha kwamba alitumia neno hilo kuyaelezea mataifa ya Afrika. Hata hivyo alikiri kwamba alitumia maneno makali akiyaeleza mataifa ya Afrika, Haiti na El Salvador alipokuwa anazungumzia wahamiaji wanaoingia Marekani. Lakini katika mkutano wake na Kagame pambizoni mwa Mkutano wa Uchumi wa Dunia mjini Davos, Trump hajaonyesha dalili zozote za majuto kuhusu tamko lake la awali kuhusu Afrika.Bw Trump ameeleza mkutano wake wa leo na Kagame kama "wa kufana sana", na kueleza nchi hizo mbili kama washirika wa kibiashara ambao wanajivunia "uhusiano mzuri sana." Ameongeza: "Ningependa kukupongeza, Bw Rais, unapochukua majukumu ya kuwa kiongozi mpya wa Umoja wa Afrika, ni heshima kubwa … najua unaenda kuhudhuria mkutano wa kwanza karibuni. Tafadhali, fikisha salamu zangu." Rais Kagame alisema wameshauriana kuhusu ushirikiano wa nchi hizo mbili, ikiwa ni pamoja na usaidizi wa Marekani kwa Rwanda katika "operesheni zake kote duniani", pamoja na masuala ya kiuchumi, biashara, uwekezaji na idadi ya watalii wa Marekani wanaozuru Rwanda, ambayo inaongezeka. Mkutano wa viongozi wa nchi wanachama wa AU utafanyika Jumapili na Jumatatu.

Latest News

Amtumia ndugu yake kutoroka jela
14 Feb 2018 14:15 - Mohamed Mnzava

Mamlaka nchini Peru zimemkamata mfungwa zaidi ya mwaka mmoja tangu atoroke jela kwa kumuacha ndugu yake pacha katika naf [ ... ]

Ukame Cape Town umekuwa 'Janga la kitaifa'
14 Feb 2018 14:05 - Mohamed Mnzava

Afrika kusini imetangaza ukame unaoshuhudiwa Cape Town - mji unao elekea kuishia bila ya hata tone la maji - kuwa janga  [ ... ]

Waziri Mwigulu azungumzia kampeni kuhusishwa na tukio la Mbunge Lissu
14 Feb 2018 13:51 - Mohamed Mnzava

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mwigulu Nchemba amewataka wanasiasa kuacha kutumia kesi ya kuumwa kwa Mbunge wa Singida [ ... ]

Other Articles

Social Media

Copyright © 2018 . Star Tv - Tanzania. All Rights Reserved.